WAZIRI
MKUU Mizengo Pinda amepokea msaada wa mabati 350 yenye thamani ya milioni 17.2
ikiwa ni mchango kutoka Mfuko wa Hifadhi ya Jamii wa GEPF kwa ajili ya ujenzi
wa shule ya msingi Kakuni iliyoko katika kijiji cha Kibaoni, Wilayani Mlele,
Katavi.
Waziri
Mkuu amepokea mchanga huo jana (Jumatatu, Mei 26, 2014) kwenye eneo la shule
hiyo wakati akiwa njiani akitokea Sumbawanga, Rukwa ambako alimwakilisha Rais
Jakaya Kikwete kwenye ibada ya kumuweka wakfu Askofu Mteule Conrad Nguvumali wa
Kanisa la Moravian Tanzania Jimbo la Rukwa.
Akitoa
taarifa fupi ya ujenzi wa shule hiyo, Katibu Tawala wa Mkoa wa Katavi, Mhandisi
Emmanuel Kalobelo alisema shule hiyo mpya inajengwa ili iwe mbadala wa shule ya
zamani ambayo alisoma Waziri Mkuu Mizengo Pinda mwishoni mwa miaka ya 50.
“Wazo
la kujenga shule hii upya lilitoka kwako wewe mwenyewe hasa kwa kuzingatia uchakavu wa majengo ya shule, ufinyu wa eneo
ilipo shule kwa sasa ukilinganisha na
wingi wa wanafunzi na mahitaji ya kielimu na kuongezeka kwa mahitaji na
miundombinu muhimu kulingana na mahitaji ya shule kwa sasa,” alisema Bw.
Kalobelo.
Bw.
Kalobelo alisema kutokana na wazo hilo, uongozi wa Serikali ya Kijiji ulitoa
ekari 66 kwa hiari yao ili shule hiyo mpya ijengwe. “Sisi kama Serikali ya Mkoa
tunakushuru kwa wazo lako hili ambapo unaendelea kuwezesha ujenzi wa Shule hii
kupitia michango ya wadau mbalimbali,” aliongeza.
Bw.
Kalobelo alisema shule hiyo itakuwa ya kwanza Kimkoa kwa kuwa na miundombinu ya
kisasa kwani kutakuwa na madarsa 14, jengo la utawala, maktaba ya wanafunzi na
walimu, vituo vya ICT viwili (kimoja cha wanafunzi na kingine cha walimu),
kumbi za mikutano mbili na bwalo la chakula.
Alitaja
vitu vingine kuwa ni viwanja vya michezo vya kisasa, nyumba za walimu tisa, vyoo
vyenye matundu 48, maji na umeme, eneo la maduka (Shopping Centre), karakana za
ufundi ushonaji nguo na viatu, useremela na ufundi makenika, shule ya awali ya
kisasa na sehemu ya shughuli za kilimo cha bustani (Elimu ya Kujitegemea).
Akiwasilisha
mchango huo, Mkurugenzi Mtendaji wa GEPF, Bw. Daudi Msangi alisema wamekabidhi
kwanza mabati 151 na kofia 40 na watakamilisha mabati mengine 200 baada ya muda
mfupi.
“Awali
tulipanga kuchangia mabati kwa ajili ya jengo la TEHAMA lakini kwa vile bado
halijaanza kujengwa, tumeamua kuchangia jengo la utawala pamoja na madarasa
mawili yaliyobakia,” alisema.
Naye
Mwenyekiti wa Kijiji cha Kibaoni, Bw. Gaston Kamine alisema wanashukuru kwa
msaada huo na wanasubiri kwa hamu kukamilika kwa ujenzi wa shule hiyo. Alisema kama
kijiji, wako tayari kutoa msaada wowote wakati wakihitajika kufanya hivyo.
Akitoa
shukrani kwa Mfuko wa GEPF, Waziri Mkuu Pinda alisema mchango walioutoa ni
msaada mkubwa sana na utachangia kukamilisha jengo la utawala ambalo ujenzi
wake umekaribia kwenye linta.
Hadi
sasa, ujenzi wa shule hiyo ambao ulianza mwishoni mwa kama jana, umekamilika
kwa kujenga madarasa 12 na mawili yatakamilika baada ya jengo la utawala
kukamilika.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni