mzindakaya
*Ataka viongozi wa dini
wasichoke kuombea amani ya Taifa
*Mzindakaya agoma
kumsamehe Mbunge wa Sumbawanga Mjini
WAZIRI
MKUU Mizengo Pinda amesema Serikali itaendelea kusimamia msimamo wake wa
kutokuwa na dini wala nchi kutokuwa na dini lakini itaendelea kuruhusu watu
wawe na dini zao.
Ametoa
kauli hiyo leo mchana (Jumapili, Mei 25, 2014) kwenye ibada ya kumuweka wakfu
Askofu Mteule Conrad Nguvumali wa Kanisa la Moravian Tanzania Jimbo la Rukwa iliyofanyika
kwenye Uwanja wa Nelson Mandela, mjini Sumbawanga.
Waziri
Mkuu ambaye alikuwa mgeni rasmi kwa niaba ya Rais Jakaya Kikwete ambaye yuko
nje ya nchi kikazi, alisema: “Leo tukiruhusu Serikali iwe na dini na tayari
katika dini zote kuna makundi madogo madogo, je wale wa upande mwingine
utawaacha wapi?”.
Pia
alitumia fursa hiyo kuwaasa viongozi wa dini nao pia waangalie wasitumbikie
kwenye mtego wa siasa na kuruhusu kanisa zima liwe la chama fulani kwani
miongoni mwa waumini wao wapo pia wapenzi wa vyama vingine.
“Kama
mtu binafsi, kiongozi wa dini anaweza kuwa mpenzi wa chama lakini kama Kanisa
tusiruhu hali hiyo,” alionya.
Aliwaomba
viongozi wa dini waendelee kuliombea Taifa na hasa waombee amani ya Taifa hili.
“Ninawasishi viongozi wa dini msichoke kuombea amani ya Taifa hili kwani amani
ikipotea kama nchi hatuna mahali pa kukimbilia.
Katika tukio jingine, Mbunge wa zamani wa jimbo la Kwela,
Mzee Chrisant Mzindakaya amekataa kumsamehe hadharani Mbunge wa sasa wa
Sumbawanga Mjini, Bw. Aeshi Hilali baada ya kupewa fursa ya kushikana mikono jukwaani
na kusameheana.
Mzee
Mzindakaya alikataa kufanya hivyo akisema yeye ni mkristu lakini hakuwa
ameandaliwa kiroho kwa ajili ya tukio hilo. “Hapa ni shughuli ya kanisa na si
mkutano wa Chama. Lazima niwe mkweli leo sijajiandaa kwa jambo hili… Mimi ni
mtu mzima, nafsi ya msamaha inahitaji maandalizi, nahitaji maandalizi ya
kiroho,” alisema.
Hata
hivyo, alikiri kwamba amekubali msamaha alioombwa na Bw. Aeshi lakini hawezi
kuutoa katika shughuli ya Kanisa. “Nilishamwambia Mwenyekiti wa CCM mkoa
aitishe mkutano, wazee wa chama wawepo na sisi wawili tuwepo kwa sababu
nimetukanwa sana kama vile sijaifanyia jambo lolote nchi hii,” alisisitiza.
“Niliwaeleza
pia waandae mikutano ya nje kule kwa wanachama ambako nilichafuliwa sana. Nikisema
nimemsamehe hapa nitakuwa mnafiki,” aliongeza.
Kwa
upande wake, Bw. Aeshi ambaye alipewa nafasi ya kwanza kuomba msamaha, alisema
anatambua kwamba bega haliwezi kukizidi kichwa na yeye kama mtoto anamuomba
msamaha Mzee Mzindakaya kwa yaliyopita ili waweze kufanya kazi pamoja na kuleta
maendeleo kwa wakazi wa jimbola Sumbawanga Mjini.
“Natambua
kuwa mimi ni mtoto na siku zote mdogo atabaki kuwa mdogo lakini naomba busara
zake ili tushirikiane kuleta maendeleo ya mkoa wetu… yaliyopita si ndwele
tugange yajayo. Nimetamka maneno haya mbele ya viongozi wa dini na mbele ya
Mungu kwa kuwa najua yuko hapa,” alisema.
Mkuu
wa Mkoa wa Rukwa, Mhandisi Stella Manyanya ndiye aliwaomba Mzee Mzindakaya na
Bw. Aeshi wapande jukwaani na kupeana mikono na kisha akawapa kila mtu fursa ya
kutoa neno.
Mhandisi
Manyanya alisema siku ya leo ni ya kipekee na akaona asipoteze fursa hiyo bali aitumie
kuwaomba viongozi hao ambao wamekuwa na uhasama wa muda mrefu wayamalize kwa
kupeana mikono hadharani.
(mwisho)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni