I: UTANGULIZI
(a)
Masuala ya jumla
Mheshimiwa
Spika,
1.
Tumekuwepo
hapa kwa takriban siku 12 katika shughuli za Mkutano wa 18 wa Bunge lako Tukufu.
Ni jambo la kumshukuru Mwenyezi Mungu mwenye wingi wa Rehema kwa kutufikisha
salama siku ya leo.
2.
Lakini
tumekutana hapa tukiwa tumeshuhudia mabadiliko katika Baraza la Mawaziri na Wenyeviti
wa baadhi ya Kamati za Kudumu za Bunge. Niruhusu nitumie nafasi hii ya awali kuwapongeza
Mawaziri na Naibu Mawaziri wote ambao wameteuliwa kushika nyadhifa mbalimbali
katika mabadiliko hayo. Aidha, napenda niwapongeze Wenyeviti watatu pamoja na
Makamu mmoja kwa kuchaguliwa kuongoza Kamati za Kudumu za Bunge ikiwemo Kamati ya
Bajeti, Kamati ya Nishati na Madini na Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala. Tunawatakia
afya njema Mawaziri, Naibu Mawaziri na Wenyeviti wote katika kutekeleza
majukumu yao mapya.
Mheshimiwa Spika,
3.
Tangu
tulipomaliza Mkutano wa 16 na 17 wa Bunge lako Tukufu, kumetokea majanga katika
sehemu mbalimbali Nchini ikiwemo mafuriko na mapigano ya Wakulima na Wafugaji
kule Morogoro, pamoja na ajali za barabarani. Naomba nitumie nafasi hii kuwapa
pole wote walioathirika na majanga, maafa na ajali za barabarani. Kwa wale waliopoteza maisha tunawaombea kwa
Mwenyezi Mungu azilaze roho za marehemu mahala pema peponi Amina.
b) Maswali
Mheshimiwa
Spika,
4.
Katika
Mkutano huu, Waheshimiwa Wabunge wamepata fursa
ya kuuliza maswali ya kawaida na yale ya papo papo kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu.
Jumla ya maswali 122 ya msingi na 313 ya nyongeza yaliulizwa na
Waheshimiwa Wabunge na kujibiwa na Serikali.
Aidha, Maswali 15 ya msingi
na 13 ya nyongeza yaliulizwa na
kujibiwa kwa utaratibu wa maswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu.
(c) Miswada
na Taarifa Mbalimbali
Mheshimiwa
Spika,
5.
Tunahitimisha Mkutano huu tukiwa tumekamilisha
kazi kubwa ya kusoma na kujadili taarifa mbalimbli za Kamati za Bunge za Kisekta
na zisizo za Kisekta. Kamati za Kisekta ambazo Taarifa zake zimewasilishwa na
kujadiliwa na Waheshimiwa Wabunge ni zifuatazo:
i)
Kamati
ya Miundombinu;
ii)
Kamati
ya Nishati na Madini;
iii)
Kamati
ya Ardhi, Maliasili na Mazingira;
iv)
Kamati
ya Kilimo, Mifugo na Maji;
v)
Kamati
ya Katiba, Sheria na Utawala;
vi)
Kamati
ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa;
vii)
Kamati
ya Masuala ya UKIMWI;
viii)
Kamati
ya Ulinzi na Usalama;
ix)
Kamati
ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa;
x)
Kamati
ya Huduma na Jamii; na
xi)
Kamati
ya Maendeleo ya Jamii.
6.
Aidha,
Bunge Lako Tukufu lilipokea na kujadili Taarifa za Kamati zisizo za Kisekta
zinazosimamia Fedha za Umma zifuatazo:
i)
Kamati
ya Hesabu za Serikali;
ii)
Kamati
ya Hesabu za Serikali za Mitaa; na
iii)
Kamati
za Bajeti.
Mheshimiwa Spika,
7.
Vilevile,
tumepokea na kujadili taarifa ya Kamati Teule ya Bunge iliyoundwa kuchunguza sababu
za migogoro baina ya Wakulima, Wafugaji Wawekezaji na Watumiaji wengine na
Ardhi Nchini.
Mheshimiwa
Spika,
8.
Katika
Mkutano huu, tulipanga na tulitarajia kujadili Muswada wa Sheria ya Usimamizi
wa Kodi wa mwaka 2014 (The Tax Administration Bill. 2014); Muswada wa Sheria ya
Takwimu wa mwaka 2013 (The Statistics Bill, 2013); na Muswada wa Sheria ya
Marekebisho ya Sheria mbalimbali (Na. 2) wa mwaka 2014, (The Written Laws
Miscellaneous Amendments (No. 2) Bill, 2014) ambao ndio pia ulihusu Muswada wa
Marekebisho ya Sheria ya Kiislamu Sura 375.
(The Islamic Law (Restatement) Act)
unaotambua Mahakama ya Kadhi.
Mheshimiwa
Spika,
9.
Hata
hivyo, hatukuweza kuijadili Miswada hiyo katika Mkutano huu, ili Kamati husika
zipate nafasi na muda wa kupitia na kutoa ushauri kwa Bunge lako Tukufu. Ni
matumaini yangu kwamba Miswada hii itapata nafasi ya kuwasilishwa na kujadiliwa
katika Mkutano ujao wa 19 wa Bunge lako Tukufu.
d) Hoja za Wabunge na
Kauli za Mawaziri
Mheshimiwa
Spika,
10.
Pamoja
na shughuli zilizopangwa katika Mkutano huu, Waheshimiwa Wabunge walipata pia
fursa ya kupokea na kujadili Hoja ya Mheshimiwa James Mbatia kuhusu kukamatwa
na Polisi kwa Mwenyekiti wa Chama cha CUF Profesa Ibrahim Lipumba kutokana na
maandamano ya Wafuasi wa Chama hicho yaliyofanyika Jijini Dar es Salaam kiyume
cha Sheria. Aidha, Serikali kupitia
Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika ilipata nafasi ya kutoa kauli ya Serikali
kuhusu kutatua changamoto za soko la Sukari Nchini.
Mheshimiwa
Spika,
11.
Nitumie
nafasi hii kuwapongeza Waheshimiwa Wabunge wote kwa kushiriki kupokea na
kujadili taarifa mbalimbali zilizowasilishwa. Napenda kuliahidi Bunge lako
Tukufu kwamba michango ya Waheshimiwa Wabunge, maoni na mapendekezo ya Kamati
zote kwa ujumla yatazingatiwa na Serikali kwa utekelezaji.
II: KILIMO
a)
Hali ya Uzalishaji na
Upatikanaji wa Chakula
Mheshimiwa
Spika,
12.
Hali
ya uzalishaji na upatikanaji wa chakula nchini kwa ujumla imeendelea kuwa ya kuridhisha
katika maeneo mengi kufuatia mavuno mazuri katika msimu wa kilimo wa 2013/2014.
Tathmini ya awali ya uzalishaji wa mazao ya chakula Nchini hadi mwezi Septemba,
2014 inaonesha kuwa uzalishaji wa mazao ya chakula katika msimu wa kilimo wa
2013/2014 ulifikia jumla ya Tani Milioni
16.0 zikiwemo Tani Milioni 9.8
za mazao ya nafaka na Tani Milioni 6.2
za mazao yasiyo ya nafaka.
13.
Katika
kipindi hicho, makadirio ya mahitaji ya chakula Nchini kwa mwaka 2014/2015
zilionesha kuwa tunahitaji Tani Milioni
12.8. Hivyo, kutokana na uzalishaji huu, Nchi ina ziada ya Tani Milioni 3.2 za chakula, na tumewezesha
kujitosheleza kwa chakula kwa Asilimia
125. Napenda kutumia fursa hii kuwapongeza Wananchi na hasa Wakulima wote
Nchini kwa kuitikia wito wa Serikali
wa Mpango wa “KILIMO KWANZA”, na
kuongeza tija katika uzalishaji, ambao umetuwezesha kupata mavuno mengi na
kupata ziada hii ya chakula. Serikali itaendelea kuweka juhudi zaidi katika
uzalishaji wa mazao ya Chakula ili kulihakikishia Taifa letu kuondokana na njaa
na aibu ya kuomba chakula kutoka nje ya Nchi.
Mheshimiwa
Spika,
14.
Tathmini
hii pia imeonesha kuwa, uzalishaji wa nafaka kwa ujumla umeongezeka kutoka Tani Milioni 7.6 msimu wa 2012/2013
hadi Tani Milioni 9.8 msimu wa
2013/2014. Kati ya Tani hizo Milioni 9.8,
Tani Milioni 6.7 ni za mahindi, Tani Milioni 1.7 ni za mchele na Tani Milioni 1.4 mtama. Kutokana na mahitaji ya nafaka kwa msimu wa
2014/2015 kuwa Tani Milioni 8.1;
Taifa lina ziada ya Tani Milioni 1.4
za nafaka. Uzalishaji wa mahindi ambayo ni chakula kikuu umeongezeka kutoka Tani Milioni 5.2 katika msimu wa
2012/2013 hadi kufikia Tani Milioni 6.7
katika msimu wa 2013/2014. Kutokana na mahitaji ya mahindi kwa mwaka 2014/2015
kukadiriwa kuwa Tani Milioni 5.2,
Taifa lina ziada ya Tani Milioni 1.5 za
Mahindi sawa na Asilimia 29.7.
Vilevile, uzalishaji wa mchele umeongezeka kutoka Tani Milioni 1.3 msimu wa 2012/2013 hadi Tani Milioni 1.7 katika msimu wa 2013/2014. Kwa vile makadirio ya
mahitaji ya mchele kwa mwaka 2014/2015 ni Tani 900,000, Taifa lina ziada ya Tani 800,000 za mchele, sawa na Asilimia 89.
b) Hali ya Akiba ya Chakula
Mheshimiwa Spika,
15.
Wakala
wa Hifadhi ya Chakula wa Taifa (NFRA) walianza ununuzi wa nafaka katika msimu
wa 2014/2015 wakiwa na akiba ya chakula ya Tani
189,493.7. Hadi kufikia tarehe 29 Januari, 2015 NFRA ilikuwa imeshanunua
jumla ya Tani 298,122.3 za nafaka
sawa na Asilimia 107.1 ya lengo la
ununuzi. Aidha, kiasi cha chakula kilichochukuliwa katika maghala hadi tarehe
29 Januari, 2015 kilikuwa Tani 29,290.5.
Jumla ya Tani 1,117.5 ziko njiani kutoka vituo vya Vijijini kwenda katika
maghala ya Wakala wa Hifadhi ya Chakula wa Taifa katika Kanda mbalimbali. Hivyo
hadi tarehe 29 Januari, 2015, akiba ya chakula katika maghala ya Wakala wa
Hifadhi ya Chakula wa Taifa ilikuwa Tani
460,175.5 zikiwepo Tani 451,589.1
za mahindi; Tani 3,939.6 za mpunga;
na Tani 4,646.8 za mtama.
c)
Changamoto ya Hifadhi
ya Nafaka
Mheshimiwa Spika,
16.
Pamoja na mvua nzuri
zilizonyesha katika msimu wa 2013/2014, ongezeko hili la uzalishaji wa chakula
limechangiwa na juhudi za Serikali za kuhimiza Wananchi kuongeza matumizi ya
zana kubwa za kilimo (Matrekta) pamoja na kutoa pembejeo za ruzuku kwa
wakulima. Aidha, bei nzuri ya kununulia mahindi ya Shilingi 500 kwa kilo iliyotumiwa na Wakala wa Hifadhi ya Chakula wa Taifa
iliwavutia wakulima wengi kupeleka mahindi yao katika vituo vya ununuzi vya Wakala
jambo lililowafanya Wakala kushindwa kununua nafaka za ziada kutoka kwa wakulima na
hivyo kusababisha kuwepo kwa malalamiko mengi kutoka kwa wakulima. Hadi kufikia
tarehe 11 Novemba 2014, uwezo wa Wakala wa kuhifadhi nafaka
katika maghala yake ulikuwa ni Tani 246,000 tu, hivyo kutokana na akiba
kubwa iliyopo sasa ya Tani 460,175.5, imewalazimu
Wakala kuhifadhi sehemu
ya akiba hiyo katika maghala mengine Vijijini, katika Taasisi za Serikali na
Sekta Binafsi; na nje ya maghala ya Wakala kwa kufunikwa na
maturubai.
d)
Mpango wa kuongeza
maghala ya Hifadhi ya Taifa
Mheshimiwa
Spika,
17.
Makadirio
ya mahitaji ya hifadhi Kitaifa kwa kipindi cha muda mfupi
ni tani 400,000; kwa kipindi cha
muda wa kati ni tani
700,000; na tani 1,000,000 kwa
kipindi cha muda mrefu. Katika
jitihada za kukabiliana na changamoto ya upatikanaji wa maghala ya
kutosha ya kuhifadhi nafaka katika maghala ya Wakala wa Hifadhi ya Chakula wa Taifa, Serikali imeandaa mpango maalum
unaotarajiwa kugharimu takriban Shilingi
Bilioni 212 wa kuongeza uwezo wa NFRA wa kuhifadhi nafaka hadi kufikia Tani 400,000 ifikapo mwaka 2015/2016. Chini
ya mpango huo, Serikali itajenga maghala au vihenge vya kisasa (Silos) katika
maeneo yenye uzalishaji mkubwa wa nafaka.
e)
Ujenzi wa Vihenge vya
Kisasa (Silos)
Mheshimiwa Spika,
18.
Kutokana
na kuwepo kwa changamoto ya ujenzi wa Silos, nilipokuwa Nchini Poland mwezi Oktoba
2014 nilipata fursa ya kukutana na Viongozi wa Serikali ya Poland pamoja na kutembelea
Kampuni ya Mtynpol inayohusika na ujenzi wa Silos,
kuhifadhi na kusindika nafaka kwa kutumia teknolojia za kisasa. Nilitumia fursa
hiyo, kumwomba Makamu wa Rais wa Chama cha Wafanyabiashara cha Poland, Bwana
Witold Karczewski ambaye pia ndiye Mwekezaji wa maghala (Silos) na Viwanda vya usindikaji Nchini Poland kutembelea Tanzania
ili kuona uwezekano wa kujenga Silos zitakazotumia
teknolojia inayoendana na mazingira ya Tanzania.
Mheshimiwa Spika,
19.
Tarehe
4 hadi 5 Oktoba, 2014; Bwana Witold alifika hapa nchini na kwa pamoja
tulitembelea maghala ya Wakala wa Hifadhi ya
Chakula wa Taifa
yaliyopo Kizota – Dodoma. Baada ya ziara hiyo, mwezi Novemba, 2014 Serikali ya
Tanzania imewasilisha maombi ya
kupata Mkopo wa masharti nafuu kutoka Serikali ya Poland. Napenda kulijulisha
Bunge lako Tukufu kuwa tayari Serikali ya Poland imepokea na kuyapitia maombi
yetu; na mwishoni mwa mwezi huu wa Februari, 2015; Wizara ya Fedha inatarajia
kukamilisha mazungumzo ya kupata mkopo huo wa masharti nafuu. Ni matumaini
yangu kuwa utekelezaji wa mradi huo utaanza mapema mwaka huu baada ya Serikali
ya Poland kuridhia maombi hayo.
f) Hali ya Usambazaji wa Pembejeo
ya Ruzuku Nchini
Mheshimiwa Spika,
20.
Kuanzia
mwaka 2003/2004 hadi mwaka 2007/2008, Serikali imekuwa ikitoa ruzuku ya
pembejeo za kilimo kwa wakulima kama fidia za gharama za usafiri ili pembejeo
hizo ziuzwe kwa bei moja Nchi nzima. Kutokana na changamoto mbalimbali za
kiutendaji, Mfumo huo ulibadilishwa na kuanzisha utaratibu wa kutumia Vocha
kati ya mwaka 2008/2009 hadi msimu wa 2013/2014.
Mheshimiwa
Spika,
21.
Mpango
huo katika kipindi hiki cha miaka kumi umewezesha uzalishaji wa mazao ya
chakula kuongezeka kutoka Tani Milioni
7.7 mwaka 2003/2004 hadi kufikia Tani
Milioni 16 mwaka 2013/2014. Ongezeko hili limechangia ongezeko la viwango
vya utoshelevu wa chakula Nchini kutoka Asilimia
88 mwaka 2003/2004 hadi kufikia Asilimia
125 mwaka 2013/2014. Aidha, uzalishaji wa zao la mahindi umeongezeka kutoka
Tani Milioni 3.2 mwaka 2003/2004 hadi
Tani Milioni 6.7 mwaka 2013/2014.
Uzalishaji wa mchele umeongezeka kutoka Tani 600,000 mwaka 2003/2004 hadi Tani Milioni 1.7 mwaka 2013/2014.
Mheshimiwa Spika,
22.
Ongezeko
la uzalishaji wa mazao hayo pamoja na sababu nyingine limechangiwa na ongezeko
la matumizi ya pembejeo zilizotokana na mpango wa ruzuku. Pamoja na mafanikio
ya mpango wa ruzuku ya pembejeo za kilimo kupitia utaratibu wa Vocha,
pamekuwepo na changamoto katika ngazi mbalimbali za utekelezaji, ikiwemo
ubadhirifu, upotevu wa Vocha na ucheleweshaji wa Vocha, hali iliyosababisha
wakulima wengi kushindwa kupata pembejeo kama ilivyokusudiwa.
g)
Mfumo mpya wa
usambazaji wa pembejeo Mwaka 2014/2015
Mheshimiwa Spika,
23.
Katika
kukabiliana na changamoto zilizopo katika Mpango wa Ruzuku ya Pembejeo kwa kutumia
vocha; na katika jitihada za kutekeleza azma ya kuwapelekea wakulima pembejeo
kwa ufanisi zaidi, Serikali katika msimu wa 2014/2015 imebuni utaratibu mpya wa
majaribio ambao lengo lake ni kuviwezesha vikundi na Vyama vya Ushirika
kuchukua mikopo ya pembejeo za kilimo kutoka Taasisi za za fedha; na vikundi
vya wakulima, VICOBA na Vyama vya Ushirika moja kwa moja kutoka katika
Makampuni ya Pembejeo.
h)
Hatua za Utekelezaji
wa Mfumo mpya wa Ruzuku za Pembejeo
Mheshimiwa Spika,
24.
Jumla
ya Kaya 946,000 zinatarajiwa
kunufaika na Mpango wa Ruzuku ya Pembejeo za Kilimo kutoka Taasisi za Fedha na
Makampuni ya pembejeo. Hadi sasa AMCOS
247 katika Mikoa ya Tabora, Kigoma,
Mbeya (Chunya) Katavi, Singida, Iringa na Shinyanga zimepata mikopo ya
pembejeo ya jumla ya Shilingi 74,737,708
kupitia Benki za CRDB. Benki ya NMB imetoa mikopo kwa vikundi sita (6)
vinavyojishughulisha na kilimo cha mpunga yenye thamani ya Shilingi Milioni 600. Kupitia Benki za Wananchi, vikundi vya wakulima 147 katika Wilaya za Mbinga,
Njombe, Mufindi, Kagera na Tandahimba vyenye wanachama 3,242 vilipata mikopo ya pembejeo yenye thamani ya Shilingi Milioni 844.4.
25.
Kwa
vile Halmashauri za Wilaya zitahusika moja kwa moja katika suala la usimamizi
wa mpango huu, na kwa vile Kamati za pembejeo za Wilaya zitakuwa chini ya
usimamizi wa Mkuu wa Wilaya, ninawaagiza Viongozi wa Mikoa na Wilaya kusimamia
kwa karibu zoezi la kuhamasisha vikundi kuchukua mikopo katika Taasisi za fedha
na vyombo vingine na kuhakikisha kuwa usambazaji wa pembejeo hizi unafanyika
ipasavyo ili tuongeze idadi ya wanufaika wa mfumo huu na kuufanya kuleta
mafanikio yaliyotarajiwa kwa manufaa ya Wananchi na Taifa kwa ujumla.
i) Mwenendo wa Malipo ya
Madeni ya Ununuzi wa Mahindi kwa Msimu wa 2014/2015
Mheshimiwa Spika,
26.
Kama
nilivyoeleza hapo awali, Wakala wa Hifadhi ya
Chakula wa Taifa
ilikuwa na kazi kubwa ya kununua nafaka kutoka kwa wakulima; vikundi vya
wakulima na wafanyabishara. Kutokana na wakulima kupewa bei nzuri; na kutokana
na wakulima kwa hiyari yao kuomba mazao yao yanunuliwe na Wakala kwa
mkopo kuepuka kuharibika, wakulima walifika kwa wingi katika vituo vya mauzo
tofauti na kiasi cha fedha ambacho Wakala walikuwa wametenga
kwa ununuzi hivyo kuliwasababishia wakulima adha kubwa.
Mheshimiwa
Spika,
27.
Hadi kufikia Mwezi
Desemba 2014 Serikali ilikuwa inadaiwa kiasi cha Shilingi Bilioni 89 za Wakulima waliouzia Wakala mahindi. Aidha,
hadi kufikia tarehe 29 Januari, 2015, Serikali ilikuwa imelipa wakulima hao kiasi
cha Shilingi Bilioni 15 na kubakiza
deni la Shilingi Bilioni 74. Katika juhudi za Serikali za kutatua
changamogo ya deni hili, Mwezi Februari 2015 Serikali inatengemea kulipa kiasi
cha Shilingi Bilioni 40 na kubakia
na deni la Shilingi Bilioni 34 ambazo
tunategemea zitalipwa kutokana na mkopo wa CRDB wa Shilingi Bilioni 15 na Bajeti ya Serikali. Aidha, Serikali pia imepanga kuuza kiasi cha Tani 175,000 kutoka katika akiba yake
ya chakula kwa Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) na wafanyabishara. Nichukue fursa hii kuwapa pole wakulima wanaoidai Serikali kwa usumbufu
wanaopata. Hata hivyo, ninapenda kuwahakikishia
kuwa wote watalipwa
stahili zao katika kipindi kifupi kijacho.
III. ELIMU
(a)
Jitihada za
Utengenezaji wa Madawati
Mheshimiwa Spika,
28.
Moja
ya changamoto tulizonazo katika kipindi hiki kwenye Sekta ya Elimu ni pamoja na
suala la madawati katika Shule za Msingi na Sekondari Nchini. Taarifa nilizo
nazo ni kuwa, hadi sasa mahitaji yetu kama Nchi ni madawati Milioni 3.3 kwa Shule za Msingi, na tayari
tunayo Madawati Milioni 2.1 sawa na Asilimia 63 ya mahitaji. Kwa maana hiyo,
tuna upungufu wa madawati Milioni 1.2 sawa na Asilimia 37. Kwa upande wa Shule
za Sekondari tunayo madawati Milioni 1.4 kati ya madawati 1.5 yanayohitajika au
Asilimia 92 ya mahitaji. Kuna upungufu wa madawati takriban 120,000 sawa na Asilimia
Nane ya mahitaji. Upungufu huo ni
kwa idadi ya wanafunzi walioko Shule za Msingi na Sekondari kwa sasa.
29.
Wakati
tunazungumzia upungufu huo wa madawati idadi ya Wanafunzi wa Shule ya Msingi na
Sekondari inaendelea kuongezeka mwaka hadi mwaka kadiri idadi ya watu
inavyoongezeka. Hivyo, kasi yetu ya kuondoa upungufu wa madawati inatakiwa kuwa
kubwa kuliko kasi ya ongezeko la wanafunzi wa Shule za Msingi na Sekondari kwa
mwaka. Ni jukumu letu wote Serikali, Sekta Binafsi pamoja na Wananchi kwa
ujumla kuondoa upungufu huo hususan katika Shule za Msingi.
Mheshimiwa Spika,
30.
Serikali
imekuwa ikichukua hatua mbalimbali za kuondoa tatizo hili la madawati. Hatua
hizo ni pamoja na kupeleka fedha za ununuzi wa madawati kutoka Serikali Kuu
kwenda kwenye Serikali za Mitaa. Aidha, kiasi cha Shilingi Bilioni 12.3
zilizotokana na fedha za fidia ya Rada zilielekezwa kwenye Halmashauri kwa
ajili ya kununulia madawati. Hadi sasa madawati ya plastiki 30,996
yameshasambazwa Nchini. Usambazaji wa madawati 61,468 ya mbao utaanza hivi
karibuni. Vilevile, Serikali imekamilisha mikataba ya kusambaza madawati
mengine ya plastiki 75,699. Tunatarajia kuwa fedha hizo za Rada zitapunguza
uhaba wa madawati kwa asilimia 5.1. Katika mwaka 2014/2015, kiasi cha Shilingi
Bilioni 1.1 kimetengwa na Halmashauri kwa ajili ya kununua madawati 152,000.
Mheshimiwa Spika,
31.
Serikali
imekuwa ikishirikiana na Taasisi za Umma, Wahisani, Sekta Binafsi na Mwananchi
mmoja mmoja katika kupunguza uhaba madawati Nchini, Nitumie nafasi hii
kuwashukuru, wote ambao wamekuwa wakichangia Sekta ya Elimu hasa katika tatizo
hili la upungufu wa madawati.
a)
Ujenzi wa Maabara
katika Shule za Sekondari.
Mheshimiwa Spika,
32.
Mtakumbuka
kuwa Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania alipokuwa kwenye ziara Mkoani Singida mwaka 2012 alielekeza kila Shule
ya Sekondari Nchini iwe ina vyumba vitatu vya maabara ifikapo tarehe 30 Novemba
2014. Tangu wakati huo hadi sasa Viongozi wa Serikali Mitaa na Tawala za Mikoa
wamekuwa wakitekeleza maelekezo hayo. Hali ya ujenzi wa vyumba vya maabara
Nchini inaonesha kuwa hadi mwezi Desemba 2014 vyumba 3,607 sawa na Asilimia 34
ya mahitaji ya vyumba 10,653 vya maabara Nchini vilikuwa vimejengwa. Aidha,
Vyumba 6,249 sawa na Asilimia 59 ya mahitaji vilikuwa vinaendelea kujengwa na
Asilimia 7 bado vilikuwa havijaanza kujengwa.
Mheshimiwa Spika,
33.
Mkoa
uliofanya vizuri katika kutekeleza maelekezo ya Mheshimiwa Rais hadi kufikia
Desemba 2014 ni Mkoa wa Njombe ambao ulifanikiwa kukamilisha ujenzi wa vyumba
vya maabara kwa Asilimia 96 ya shule za sekondari zilizopo Mkoani humo. Mkoa wa
Ruvuma nao ulikamilisha ujenzi kwa Asilimia 81, ukiwa ni Mkoa wa pili Kitaifa.
Napenda kutumia fursa hii kuipongeza Mikoa hii miwili kwa kutekeleza vizuri
maelekezo ya Mheshimiwa Rais. Imeonesha mfano mzuri katika kutekeleza maelekezo
ya Kiongozi wetu wa Nchi.
Mheshimiwa Spika,
34.
Katika
zoezi hili Mkoa wa Morogoro ulikuwa Mkoa wa tatu ambao ulijitahidi kujenga
vyumba vya madarasa kwa kufikia kwa asilimia 53 ya mahitaji. Mikoa 22 iliyobaki haikuweza kufikia asilimia
50 ya lengo kwa kipindi chote cha mwaka 2012 – 2014. Kati ya Mikoa hiyo ambayo
haikuweza kufika hata robo ya lengo (Asilimia 25) katika kipindi tajwa cha
takribani miaka mitatu ni Mikoa sita; nayo ni Mtwara (Asilimia 21), Lindi
(Asilimia 20), Tabora (Asilimia 17), Dodoma (Asilimia 12), Rukwa (Asilimia 11)
na Kigoma (Asilimia 10). Tunaweza kusema hii ndiyo Mikoa ya mwisho katika
kutekeleza agizo la Rais. Mikoa 16
ambayo sikuitaja hapa iko katika kundi la Asilimia kati ya 26 hadi 49.
Mheshimiwa Spika,
35.
Mheshimiwa
Rais katika hotuba yake kwa Wananchi ya
tarehe 31 Desemba 2014 aliongeza miezi sita zaidi hadi Juni 2015 kwa wale ambao
hawajakamilisha ujenzi wa maabara hizo ili waweze kukamilisha. Ni matarajio ya
Mheshimiwa Rais kuwa muda huo unatosha kwa kila Sekondari iliyopo Nchini kuwa
na vyumba vitatu vya maabara na aliweka bayana kuwa
hakusudii kuongeza tena muda baada ya
muda huo kupita yaani Juni 2014. Hivyo, ninawataka Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa
Wilaya, Mameya, Wenyeviti na Wakurugenzi Watendaji wa Halmashauri za Wilaya na
Miji Nchini kuhakikisha maagizo haya yanatekelezwa. Aidha, ninatoa rai kwa Waheshimiwa Wabunge na
Madiwani kutoa msukumo stahiki katika utekelezaji wa maagizo haya kwa maslahi
ya Taifa letu.
36.
Kwa
upande wa Serikali, Ofisi ya Waziri Mkuu - TAMISEMI haina budi kuhakikisha
agizo hili la Mheshimiwa Rais linatekelezwa ndani ya muda uliotolewa. Aidha,
katika kufanya hivyo wahakikishe kuwa vyumba vya maabara vinavyojengwa vina
ubora stahiki na vinalingana na thamani ya fedha zilizotumika. Ubadhirifu wa
aina yoyote usipewe nafasi na watakaobainika kuhusika wachukuliwe hatua za
kisheria mapema. Nitapenda OWM - TAMISEMI waendelee kufuatilia suala hili na
kunipa taarifa mara kwa mara.
IV: SEKTA YA NISHATI
a)
Hatua iliyofikiwa
ya Upatikanaji wa Nishati Vijijini
(Miradi ya REA)
Mheshimiwa Spika,
37.
Serikali imedhamiria
kuimarisha na kuongeza kiwango cha huduma za upatikanaji wa Nishati ya
Umeme Vijijini ili kujenga msingi wa
uchumi imara na wa kisasa wa Taifa linalojitegemea. Moja ya hatua
zinazochukuliwa ni utekelezaji wa Mpango Kabambe wa usambazaji Umeme Vijijini.
Mheshimiwa Spika,
38.
Ili kufikia azma hiyo,
Wakala wa Nishati Vijijini umeanza kutekeleza Mradi Kabambe wa Awamu ya Pili
unaohusisha usambazaji wa umeme Vijijini katika Mikoa yote ya Tanzania Bara.
Mradi huu unahusisha ujenzi wa Vituo 6 vya
kupoozea umeme na njia ya kusambaza umeme kwenye maeneo yenye msongo wa 33kV yenye urefu wa Kilomita 15,000. Vilevile, utahusisha ujenzi wa
njia za kusambaza umeme yenye msongo wa kilo-Volti 400 zenye urefu wa Kilomita 8,000
na ufungaji wa Vipooza Umeme 3,300.
Mradi huu utakapokamilika utakuwa umeunganisha Wateja wa awali takriban 250,000 katika Vijiji 1,142. Mradi huu unafuatia
baada ya kukamilika kwa zaidi ya Asilimia 80
ya Mradi Kabambe wa Awamu ya Kwanza ambapo Wateja 17,688 wameunganishwa kwenye miundombinu ya usambazaji wa umeme
Nchini.
Mheshimiwa Spika,
39.
Mradi Kabambe wa Awamu
ya Pili unakadiriwa kugharimu
Shilingi Bilioni 881. Hadi sasa
takriban Shilingi Bilioni 278 zimelipwa
kwa Wakandarasi ikiwa ni malipo ya awali ya Asilimia 10 na gharama za kununua vifaa na hati za dhamana zenye jumla ya
Shilingi Bilioni 439 kwa Miradi yote
35 zimefunguliwa.
Mheshimiwa Spika,
40.
Kutokana na juhudi
za Serikali za kuongeza kasi ya kuunganisha umeme Vijijini ambazo zimechochewa
na kupunguza gharama za kuunganisha umeme kwa wananchi hasa waishio Vijijini
idadi ya Watanzania waliounganishiwa umeme imeongezeka kutoka Asilimia 2.5 kwa Mwaka 2007 hadi Asilimia 18.4 kwa Mwaka 2010 na kufikia Asilimia
24 kwa Mwaka 2014.
b)
Utekelezaji
wa Mradi wa ujenzi wa Bomba la Gesi
Mheshimiwa Spika,
41.
Kuanzia
mwaka 2013 Serikali ilianza kutekeleza Mradi wa ujenzi wa Bomba la Gesi kutoka
Mtwara na mitambo ya kuchakata na kusafisha gesi unaendelea vizuri. Mpaka
kufikia mwezi Oktoba, 2014 ujenzi wa bomba ulikuwa umefikia Asilimia 97 na ule wa mitambo ulikuwa umefikia
Asilimia 84. Kwa wastani mradi mzima
sasa umekamilika kwa Asilimia 92.
Matarajio ni kumalizika kwa ufungaji wa mitambo yote na kuanza majaribio ya
awali. Mara majaribio yote ya miundombinu yatakapokamilika, miundombinu hii
itakabidhiwa kwa Shirika la Maendeleo ya Petroli (TPDC) kwa uendeshaji. Zoezi
hilo linatarajiwa kufanyika mwezi Juni, 2015.
Mheshimiwa Spika,
42.
Ili
kujiandaa kunufaika na upatikanaji wa Gesi Asilia, TPDC imeanzisha Kampuni yake
Tanzu (GASCO) ambayo imepewa majukumu yote ya kumiliki miundombinu yote ya
usafishaji, usafirishaji na usambazaji wa gesi asilia hapa nchini pamoja na
kukusanya gesi kutoka vyanzo mbalimbali. Ili kufanikisha azma hii ya Serikali,
tayari GASCO kupitia TPDC imeajiri Wafanyakazi wapya wapatao 120 kwa ajili ya mitambo ya kusafisha
gesi na wengine 50 kwa ajili ya
kuendesha bomba la gesi.
Mheshimiwa Spika,
43.
Manufaa
mengine yatakayopatikana kutokana na upatikanaji wa
Gesi Asilia ni kupata
umeme wa uhakika
na matumizi viwandani, magari na
majumbani. Aidha, Nchi itaokoa Dola za Marekani Bilioni Moja (sawa na Shilingi
za Tanzania Trilioni 1.6) kwa mwaka
kutokana na mitambo iliyopo nchini kutumia gesi asilia badala ya mafuta. Faida
nyingine za mradi mpya ni pamoja na ajira katika mitambo itakayojengwa Madimba
na Songo Songo kwani kila mtambo utahitaji wastani wa Wafanyakazi 60. Pia, mradi utatoa ajira katika
Sekta zote na hususan za Afya, Elimu, Maji, Usafiri pamoja na huduma nyingine
za Kijamii zitakazohitajika katika maeneo husika. Natoa wito kwa Wananchi wote kulinda
miundombinu ya Gesi Asilia ambayo inajengwa kwa gharama kubwa. Aidha,
nawahimiza Wakandarasi wa Mradi wa Bomba la Gesi kukamilisha ujenzi kwa muda
uliopangwa.
V: UCHAGUZI WA SERIKALI ZA MITAA
a)
Matokeo ya Uchaguzi
wa Serikali za Mitaa
Mheshimiwa
Spika,
44.
Uchaguzi
wa Mamlaka za Serikali za Mitaa
uliofanyika Nchini tarehe14 Desemba 2014 ulihusisha uchaguzi wa Wenyeviti wa Vijiji 12,261, Wenyeviti wa Vitongoji 63,319, Wenyeviti wa Mitaa Mijini 3,884, Wajumbe wa Serikali
za Vijiji/Mitaa na Wajumbe wa Viti Maalum. Jumla ya watu 8,137,974 sawa na asilimia
69 ya watu waliojiandikisha kupiga kura walijitokeza kupiga kura. Vyama vya
Siasa 17 sawa na asilimia 81 ya Vyama vyote vyenye
usajili wa kudumu vilishiriki kwenye uchaguzi huu.
45.
Taarifa
ya matokeo inaonesha kwamba katika nafasi ya Wenyeviti wa Vijiji, CCM kilishinda
kwa asilimia 79.4, CHADEMA asilimia 15.1 na CUF asilimia 4.6. Vyama vingine kwa ujumla
vilipata asilimia 0.9. Matokeo ya Wenyeviti wa Vitongoji yanaonesha
kuwa CCM imeshinda kwa asilimia 79.3,
CHADEMA asilimia 15.6, CUF asilimia 4.3 na vyama vingine vilipata asilimia 0.8. Nafasi za Wenyeviti wa Mitaa CCM kilishinda
kwa asilimia 66.5, CHADEMA asilimia 25.4, CUF asilimia 6.8 na vyama vingine vilipata kwa asilimia 1.3. Matokeo ya
Wajumbe wa Serikali za Vijiji/Mitaa ni kuwa CCM ilipata asilimia 79.3, CHADEMA asilimia
15.7, CUF asilimia 4.3 na Vyama
vingine vilipata asilimia 0.7. Kuhusu matokeo ya Wajumbe wa Viti Maalum ni
kuwa CCM walipata asilimia 82.1,
CHADEMA asilimia 13.7, CUF asilimia 3.5 na Vyama vilivyobaki navyo
vilipata asilimia 0.7.
b)
Changamoto
Zilizojitokeza
Mheshimiwa Spika,
46.
Pamoja
na mafanikio yaliyopatikana wakati wa uchaguzi huo, zipo changamoto
zilizojitokeza katika mchakato mzima wa upigaji kura. Hii ni pamoja na kuwepo kwa vurugu siku za
uchaguzi, wagombea kufariki au kujitoa, ukosefu wa umakini katika usimamizi na
ucheleweshaji wa vifaa vya kupigia kura. Kutokana na kasoro hizo asilimia 1.2 ya maeneo yaliyostahili
kupiga kura bado hawajapiga kura. Hata hivyo, Ofisi ya Waziri Mkuu TAMISEMI
wamejipanga vizuri kuhakikisha kwamba uchaguzi wa maeneo yaliyobaki na tathmini
yake unakamilika mapema iwezekanavyo.
47.
Aidha,
kutokana na baadhi ya Wakurugenzi wa Halmashauri kuonesha udhaifu katika
kusimamia uchaguzi huo, Serikali ilichukua hatua ya kutengua uteuzi wa
Wakurugenzi sita (6) ambao ni Mkurugenzi wa Mkuranga, Kaliua, Kasulu,
Serengeti, Sengerema na Bunda. Vilevile, wapo Wakurugenzi waliosimamishwa kazi
ili kupisha uchunguzi wa makosa yao wakiwemo Wakurugenzi wa Hanang’, Mbulu,
Ulanga, Kwimba na Manispaa ya
Sumbawanga.
Wapo pia, Wakurugenzi
waliopewa “ONYO KALI” ambao ni Wakurugenzi wa Rombo, Busega na Muheza.
Wakurugenzi waliopewa “ONYO” pekee ni wa Manispaa ya Ilala, Hai, na Mvomero.
Watumishi wa ngazi za chini pia walichukuliwa hatua na Halmashauri ambazo ni
mamlaka zao za nidhamu. Utekelezaji wa hatua hizi utasaidia kupeleka ujumbe kwa
wale wote ambao watashindwa kutoa usimamizi thabiti kwenye chaguzi zijazo.
c)
Pongezi na Shukurani
kwa Wananchi
Mheshimiwa Spika,
48.
Kwa
kuzingatia mchakato mzima wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka 2014, naomba
uniruhusu nitumie fursa hii kushukuru na kuwapongeza Wananchi wote walioshiriki
na hivyo kufanikisha Uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2014. Nipongeze pia Vyama vyote vya Siasa
vilivyojitokeza kugombea nafasi mbalimbali katika uchaguzi huo. Kipekee kabisa niwapongeze Viongozi na
Wanachama wote wa Chama cha Mapinduzi kwa ushindi mkubwa na wa kishindo katika
maeneo yote kuanzia nafasi za Vijiji, Vitongoji, Mitaa, Wajumbe wa Serikali za
Mitaa/Vijiji na Viti Maalum.
VI: HALI YA MAENDELEO YA ZANZIBAR
Mheshimiwa
Spika
49.
Tarehe
10 Januari, 2015 nilibahatika kuhudhuria katika sherehe ya uwekaji jiwe la
msingi katika Shule ya Sekondari ya Kibuteni Mkoa wa Kusini Unguja. Ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Miaka 51 ya
Mapinduzi ya Zanzibar. Shule ya Sekondari ya Kibuteni (Unguja) ambayo nilikwenda
kuiwekea jiwe la msingi pamoja na shule nyingine ya Mkanyageni – Pemba
zinajengwa kwa ushirikiano na Benki ya Kiarabu kwa Maendeleo ya Afrika (BADEA)
ambapo BADEA imetoa mkopo wa Dola za Kimarekani Milioni Sita na Serikali ya
Zanzibar imatoa Dola 600,000 ambazo ni Asilimia 10 ya gharama zote. Gharama za ujenzi
kwa fedha za kitanzania inatarajiwa kufikia Shilingi Bilioni 3.0.
50.
Ujenzi
wa Shule hiyo ya kisasa ni mwendelezo wa juhudi za Serikali ya Mapinduzi ya
kusukuma maendeleo ya Elimu katika sehemu zote za Zanzibar. Aidha, Shule hii ni
miongoni mwa Shule za Sekondari 27 zilizojengwa katika kipindi cha Serikali ya
Awamu ya Saba inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein ambapo Shule 19
zimekamilika na 18 kati ya hizo zimekwisha funguliwa.
Mheshimiwa Spika,
51.
Chini
ya mkopo wa Benki Kuu ya Dunia Skuli tatu za Sekondari zimefanyiwa ukarabati
mkubwa, kampasi mpya ya Chuo cha Ualimu cha Benjamini William Mkapa huko Pemba
imejengwa, madawati na vitabu vya ziada na kiada, vifaa vya maabara na kompyuta
vimenunuliwa. Pia, mafunzo ya Ualimu kazini yameendeshwa kwa muda wa miaka
mitano. Mradi huo umegharimu Dola Milioni 48 ambapo Dola Milioni 42
zimetolewa na Benki ya Dunia na Dola Milioni sita ni mchango wa Serikali.
Mheshimiwa Spika,
52.
Wakati
tunaadhimisha miaka 51 ya Mapinduzi, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza
la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein alieleza mafanikio
yaliyopatikana Zanzibar baada ya utekelezaji wa Dira 2020, MKUZA II, Ilani ya
Uchaguzi Mkuu ya CCM ya mwaka 2010 – 2015 na Malengo ya Milenia. Miongoni mwa mafanikio muhimu yaliyopatikana
ni kukua kwa uchumi ambapo kuanzia mwaka 2010 hadi 2014 Pato la Taifa
limeongezeka kutoka Shilingi Bilioni 942.3 mwaka 2010 hadi Shilingi Bilioni 1,442.8 mwaka 2013 sawa na Asilimia 53.0. Aidha, katika kipindi hicho uchumi wa
Zanzibar ulikua kutoka Asilimia 6.4 mwaka 2010 hadi kufikia Asilimia 7.4 mwaka
2013. Pato la Mtu Binafsi nalo limeongezeka
kwa wastani wa Asilimia 38 kutoka Shilingi 778,000 mwaka 2010 na kufikia
Shilingi milioni 1.1. mwaka 2013. Kwa mwaka 2014 kasi ya kupanda kwa bei za bidhaa
na huduma (Mfumuko wa Bei) ilibaki katika wastani wa tarakimu moja ya Asilimia
5.6, ikilinganishwa na 6.1 kwa mwaka 2010.
Mheshimiwa Spika,
53.
Mafanikio
yanaonekana pia katika ukusanyaji wa mapato ambapo, katika miaka minne
2006/2007 hadi 2009/2010, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ilikusanya mapato ya
Shilingi Bilioni 484, ikilinganishwa na Shilingi Bilioni 997 zilizokusanywa
katika kipindi cha 2010/2011 mpaka 2013/2014. Takwmu hizi zinaonesha ongezeko
la Asilimia 106.
Mheshimiwa Spika,
54.
Katika
kuimarisha mazingira ya biashara kwa kushirikiana na Sekta Binafsi, Zanzibar
imeweza kusafirisha bidhaa zenye thamani ya Shilingi Milioni 94,235.8 kwa mwaka
2014 kutoka bidhaa zenye thamani ya Shilingi 87,799.6 kwa mwaka 2013, sawa na
ongezeko la Asilimia 7.3.
55.
Kwa
upande wa Sekta ya Utalii, idadi ya Watalii imeongezeka kutoka Watalii 132,836
mwaka 2010 na kufikia Watalii 274,619 mwaka 2014. Hili ni ongezeko la Asilimia 107. Katika elimu idadi ya Shule za maandalizi
imeongezeka kutoka Shule 238 mwaka 2010 hadi 279 mwaka 2014, ongezeko hili ni
sawa na Asilimia 17. Shule za Msingi
zimeongezeka kutoka 299 mwaka 2010 hadi 359 mwaka 2014 ongezeko la Asilimia
20. Shule za Sekondari zimeongezeka
kutoka 194 mwaka 2010 hadi Shule 210 mwaka 2014. Ongezeko hili ni sawa na Asilimia Nane (8%).
Idadi ya Wanafunzi katika Vyuo Vikuu imeongezeka kutoka 3,624 mwaka 2010 hadi
6,038 mwaka 2014. Ongezeko hili ni sawa
na Asilimia 67.
Mheshimiwa Spika,
56.
Katika
Seka ya Afya, idadi ya Wataalam wa Afya imeongezeka kutoka 3,634 mwaka 2010
hadi kufikia 4,618 mwaka 2014. Katika
kutoa huduma za maji safi na salama, baadhi ya maeneo yamefikisha Asilimia 87.7
ya mahitaji halisi katika Mkoa wa Mjini Magharibi Kaskazini Unguja Asilimia
71.7, Kusini Unguja 76.4 Kaskazini Pemba, Asilimia 56.4 na Kusini Pemba
Asilimia 74.1.
57.
Mafanikio
yapo pia na yanajionesha katika Sekta zingine zote kama vile Barabara,
usafirishaji na uimarishaji wa Miundombinu ya Bandari, Viwanja vya Ndege,
Kilimo, Ardhi, Upatikanaji wa Umeme, Sekta ya Mifugo na Uvuvi.
Mheshimiwa Spika,
58.
Nimeamua
kuyasema mafanikio haya kuonesha hatua iliyofikiwa kutokana na juhudi za
Serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika kujenga uchumi imara wa watu wake.
Napenda nichukue nafasi hii kumpongeza kwa dhati Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti
wa Baraza la Mapinduzi Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein na Wananchi wote wa
Zanzibar kwa jinsi wanavyoshirikiana katika kuhakikisha wanapiga hatua ya
maendeleo ya kukuza uchumi wa Zanzibar. Pamoja na pongezi hizi ni matumaini
yangu kwamba Wananchi wa Zanzibar wataendeleza ushirikiano uliopo chini ya
uongozi wa Dkt, Ali Mohamed Shein katika kukuza uchumi wa Nchi yao.
VII: HITIMISHO
Mheshimiwa
Spika,
59.
Kama
ilivyo ada, naomba nitumie nafasi hii kuwashukuru wote waliosaidia kufanikisha mkutano
huu. Nikushukuru wewe Mheshimiwa Spika, kwa kutuongoza vizuri na kwa busara kubwa.
Niwashukuru Wenyeviti wa Bunge kwa kazi nzuri ya kuongoza vikao vya Bunge
lako Tukufu. Kipekee niwatambue Mheshimiwa Lediana Mng’ong’o na Mheshimiwa
Kidawa Salehe ambao wamekalia kiti kwa mara ya kwanza lakini kwa weledi mkubwa Hongereni sana!!.
60.
Niwashukuru
tena Wenyeviti wa Kamati za Kudumu za Bunge za Kisekta na zisizo za Kisekta kwa
kuwasilisha taarifa za Kamati zao vizuri.
Aidha, niwashukuru tena Waheshimiwa Wabunge kwa kazi nzuri ya kujadili
taarifa hizo na kwa michango mbalimbali wakati wa Mkutano huu. Mapendekezo ya
Kamati zote tuliyokubaliana tumeyaweka pamoja ili kupata urahisi wa
kuyatekeleza. Tunaomba Waheshimiwa
Wabunge wote wawe na nakala ya mapendekezo hayo kwa ajili ya ufuatiliaji.
Mheshimiwa
Spika,
61.
Nitumie
nafasi hii pia kumshukuru Katibu wa Bunge na Wasaidizi wake wote kwa kazi nzuri
ya kuhakikisha mkutano huu unakamilisha shughuli zake kama ilivyopangwa. Niwashukuru
Wataalam wote wa Serikali na Taasisi zake ikijumuisha Taasisi za Sekta Binafsi,
kwa misaada ya Kitaalam na huduma mbalimbali za kufanikisha Mkutano huu.
62.
Niwashukuru
pia Waandishi wa Habari kwa kazi nzuri walizofanya kuhakikisha kuwa taarifa za
majadiliano na maamuzi mbalimbali ya hapa Bungeni zinawafikia Wananchi. Niwashukuru
Madereva kwa kazi nzuri waliyofanya ya kuwasafirisha kwa usalama Waheshimiwa
Wabunge, Viongozi mbalimbali, Wataalam na Wasaidizi wote walioshiriki katika
Mkutano huu.
Mheshimiwa
Spika,
63.
Nimalizie
kwa kuwatakia wote safari njema mnaporejea kwenye maeneo yenu ya kazi na katika
majimbo yenu. Ninaamini kwamba,
Mwenyezi Mungu atatulinda na kutuweka salama sote kama tulivyo hadi kukutana
tena katika Mkutano ujao.
64.
Baada ya kusema hayo, naomba sasa kutoa Hoja
kwamba, Bunge lako Tukufu liahirishwe hadi tarehe 17 Machi, 2015 saa 3:00 Asubuhi litakapokutana katika Mkutano wa 19 kwenye Ukumbi huu hapa Dodoma.
Mheshimiwa
Spika,
65.
Naomba
kutoa Hoja.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni