MGEJA AMTAKA DR SLAA KUACHA SIASA ZA KITOTO ZA KUMSAKAMA KINANA
Mwenyekiti
wa Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Shinyanga Khamis Mgeja amemtaka Katibu
Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Dr, Wilbroad Slaa
kuacha siasa za kitoto kwa kumsakama Katibu Mkuu wa CCM Abdulrahman
Kinana kuacha kufanya vikao na Watumishi wa Umma na kuangalia miradi ya
maendeleo pamoja na kuizindua.
Mgeja
aliyasema hayo wakati akiongea na Waandishi wa habari ofisini kwake
mkoani Shinyanga kujibu kauli ya Katibu wa CHADEMA aliyonukuliwa
alipokuwa akisema katika mikutano mbalimbali ya hadhara inayofanywa na
UKAWA katika maeneo mbalimbali hapa nchini hususani katika Mikoa ya
Arusha Iringa na Manyara.
Dr, Slaa alinukuliwa akisema kuwa katika ziara ya Katibu Mkuu wa CCM
Abdulrahman Kinana Mkoani Tabora alikutana Walimu huku akijua kuwa
hakupaswa kufanya kitendo hicho kwani kinyume cha sheria na pia
alizindua miradi mbalimbali ya Serikali.
Dr, Slaa aliendelea kuhoji kuwa Katibu Mkuu huyo wa CCM amepata wapi
mamlaka ya kuzindua miradi ya Maendeleo iliyochangiwa na Wananchi huku
akijua CCM haijachangia kitu chochote ila ni Serikali ndiyo
iliyotekeleza miradi hiyo.
Dr Slaa alisema kuwa kitendo hicho anachokifanya Katibu Mkuu huyo wa
CCM na viongozi wenzake wa Chama hicho kushiriki katika kuzindua miradi
ya maendeleo, atatangaza kama ni janga la kitaifa.
“Kitendo kinachofanywa na Katibu Mkuu wa CCM cha kushiriki katika
kuzindua miradi ya Maendeo sisi tutatangaza kama ni janga la kitaifa na
kumtaka Rais Jakaya Kikwete kuzuia kwa muda wa siku tatu la sivyo na
sisi tutaanza kukutana na Watumishi wa Umma”, Alinukuliwa Dr, Wilbroad
Slaa.
Kufuatia hali hiyo Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Shinyanga
Khamis Mgeja alisema kuwa Dr, Wilbroad Slaa anamuonea wivu katibu Mkuu
wa CCM Abdulrahman Kinana kwa kazi nzuri na mafanikio ya kimaendeleo ya
kukagua Ilani ya Chama cha Mapinduzi inavyotekelewa na Serikali yake.
Alisema kuwa Dr, Slaa na Wenzake watambue kuwa Chama cha Mapinduzi
ndicho kilichofunga mkataba na Wananchi katika kipindi cha uchaguzi cha
mwaka 2010/2015 kwa kupewa ridhaa ya kuongoza, kusimamia na kuleta
maendeleo kupitia Serikali na kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo kwa
muda huo cha kipindi cha miaka mitano.
Pia alimtaka kiongozi huyo na wapinzani wenzake kutambua kuwa hata
mtoto mdogo wa darasa la pili anatambua nini maana uchaguzi na
kukabidhiwa dhamana ya kuongoza nchi na kuongeza kuwa analolifanya
Katibu Mkuu wa CCM na viongozi wenzake wa CCM kuwa wapo sahihi kwa
mujibu wa dhamana waliokabdhiwa na Wananchi.
“Chama cha Mapinduzi kuisimamia Serikali yake sio dhambi kwani sawa na
Mwenye shamba kukagua eneo lake na Mfugaji kukagua mifugo yake na tajiri
wa mabasi kukagua mabasi yake kama yanafanya kazi na kuhudumia vizuri
wateja wake”,
“Nawashangaa Wapinzani kwa kauli zao za kujichanganya mbona Serikali
ikifanya vibaya wanakuwa wa kwanza kulaumu na kusema Serikali ya CCM
haijawatendea haki watanzania lakini ikifanya vizuri kama hivi sasa
inapowaletea maendeleo wanachi wanakataa kuwa sio Serikali ya CCM”,
Aliongeza Mgeja.
Mgeja alifananisha lawama za kumlaumu Katibu Mkuu Kinana na Chama kwa
ujumla kutimiza majukumu yake ya kuisimamamia Serikali yake
iliyokabidhiwa ridhaa na Wanachi kuiongoza ni kama kelele za chura ama
mtu mzima kumtishia Nyau na kamwe katibu Mkuu hataacha kufanya kazi yake
na kutimiza majukumu ya chama kuisimamia Serikali.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni