Msafara
wa watu 30 wa Taifa Stars unaojumuisha wachezaji, benchi la ufundi na viongozi
unaondoka kesho alfajiri (Mei 29 mwaka huu) kwenda Harare, Zimbabwe kwa ajili
ya mechi ya marudiano ya michuano ya Afrika.
Mechi
hiyo itachezwa Juni Mosi mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa jijini Harare, Taifa
Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager itatua jijini humo saa 5
asubuhi kwa ndege ya Kenya Airways.
Msafara
wa Taifa Stars ambayo ambayo jana (Mei 27 mwaka huu) ilicheza mechi ya kujipima
nguvu na Malawi na kushinda bao 1-0, na utarejea nchini Juni 2 mwaka huu
unaongozwa na Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Jamal
Malinzi.
Wakati
huo huo, mechi ya kirafiki kati ya Taifa Stars na Malawi (Flames) iliyochezwa
Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam imeingiza sh. 8,380,000 kutokana na watazamaji 1,504
waliokata tiketi kushuhudia pambano hilo.
Mgawo
ulikuwa kama ifuatavyo; Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) sh. 1,278,305.08,
gharama za kuchapa tiketi sh. 225,600, gharama za uwanja sh. 1,031,414.24,
gharama za mechi sh. 1,375,218.98 na TFF/Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania
(TFF) sh. 4,469,461.69.
MWAMBUSI KOCHA
BORA VPL 2013/2014
Kocha
Mkuu wa timu ya Mbeya City, Juma Mwambusi ameshinda tuzo ya kocha bora wa Ligi
Kuu ya Vodacom (VPL) kwa msimu wa 2013/2014.
Hafla
ya kukabidhi tuzo kwa washindi mbalimbali ilifanyika jana (Mei 27 mwaka huu)
jijini Dar es Salaam, ambapo mgeni rasmi alikuwa Rais wa Shirikisho la Mpira wa
Miguu Tanzania (TFF).
Mbali
ya tuzo hiyo, Kocha Mwambusi ambaye hivi sasa yuko nchini Sudan na timu yake
kwenye michuano ya Nile Basin alipata pia zawadi ya kitita cha sh. milioni 7.8.
Aliyeshinda
tuzo ya kipa bora ni Hussein Shariff wa Mtibwa Sugar aliyepata sh. milioni 5.2
wakati Amisi Tambwe wa Simba aliibuka na tuzo ya mfungaji bora. Tambwe naye
alipata sh. milioni 5.2.
Mchezaji
bora wa VPL kwa msimu wa 2013/2014 ni Kipre Tchetche wa Azam FC aliyejipatia
sh. milioni 5.2. Tuzo ya refa bora imetwaliwa na Israel Mujuni aliyezawadiwa
sh. milioni 7.8.
Yanga
iliyoshika nafasi ya pili kwenye ligi na kupata sh. milioni 37, pia ilipata sh.
milioni 16 baada ya kushinda tuzo ya timu yenye nidhamu ya hali ya juu. Sh.
milioni 21 za mshindi wa nne zilikwenda kwa timu ya Simba.
Mabingwa
wapya wa VPL, Azam FC walipata sh. milioni 75 wakati Mbeya City ilipata sh.
milioni 26 kwa kushika nafasi ya tatu.
RAIS MALINZI ATUMA
RAMBIRAMBI MSIBA WA KOCHA
Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Jamal
Malinzi amemtumia salamu za rambirambi Rais wa Chama cha Mpira wa Miguu Zambia
(FAZ), Kalusha Bwalya kutokana kifo cha Kocha wa timu ya Nkana FC, Masauso
Mwale.
Amesema amepokea kwa masikitiko taarifa za kifo cha ghafla
cha Kocha Mwale, na kuongeza kuwa msiba huo si pigo kwa Zambia pekee bali
Afrika kwa ujumla kwa vile ni mfano wa kuigwa kwa makocha wazalendo
waliozipatia mafanikio makubwa klabu za Afrika.
Rais Malinzi amemuomba Rais Bwalya kutuma salamu zake
za rambirambi kwa familia ya Mwale, na kuitaka kuwa na moyo wa uvumilivu katika
kipindi hiki kigumu cha msiba huo mzito kwao.
Mwale (51) alifariki mwishoni mwa wiki kwa ajali ya
gari aliyokuwa akiendesha katika barabara ya Kitwe- Ndola akienda kambini
kujiunga na timu yake kwa ajili ya maandalizi ya mechi ya Kombe la Shirikisho
dhidi ya Sewe San Pedro ya Ivory Coast.
BONIFACE WAMBURA
OFISA HABARI NA MAWASILIANO
SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA (TFF)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni