Watumishi wa umma na washiriki wa Kongamano la Miaka 50 ya Muungano katika Utumishi wa Umma wakimfuatilia kwa makini mgeni rasmi, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Mhe. Hawa Ghasia (hayumo katika picha) wakati wa ufunguzi wa kongamano hilo katika ukumbi wa kimataifa wa Mwl. Nyerere leo, jijini Dar es Salaam. |
Mgeni rasmi Waziri wa
Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Mhe. Hawa Ghasia (katikati), akiwa katika picha ya
pamoja na washiriki wa Kongamano la Miaka 50 katika Utumishi wa Umma baada ya kufungua rasmi
kongamano hilo la siku mbili Juni 19 na 20 katika ukumbi wa kimataifa wa Mwl.
Nyerere, jijini Dar es Salaam. Lengo la kongamano ni kujadili maada mbalimbali
zinazohusu utumishi wa umma. (Picha na Lorietha Laurence).
|
SERIKALI
imewataka wananchi kuzingatia taratibu za kimsingi zinazopaswa kufuatwa na mteja wakati wa
ufuatiaji na utoaji wa huduma mbalimbali zinazotolewa na watoa huduma katika
sekta ya Utumishi wa Umma nchini.
Rai
hiyo imetolewa leo tarehe (19. Juni, 2014) na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri
Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Hawa Ghasia wakati
alipokuwa akifungua kongamano la Wiki ya Utumishi wa Umma Jijini Dar es Salaam.
Waziri
Ghasia alisema katika utoaji wa huduma za umma, mwananchi ambaye ndiye mteja
mkuu katika utumishi wa umma ana wajibu wa kuwasilisha taarifa muhimu
zitakazoombwa na mtoa huduma wa sekta ya umma, na mwananchi atapaswa
kuziwasilisha kama sehemu ya udhibitisho wa kutolewa kwa huduma husika.
“Kwa
mfano mwananchi anayehitaji huduma ya cheti cha kuzaliwa kwa mtoto wake
atapaswa kuwasilisha kadi ya hospitali, ambayo itaombwa na mhudumu wa afya,
hivyo ni wajibu wa wananchi kutimiza kigezo hicho kama sharti la msingi la
kupatiwa huduma hiyo” alisema Waziri Ghasia.
Akifafanua
zaidi alisema ni dhahiri zipo changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta ya umma
na zipo zinazofanyiwa kazi na baadhi yake zinazohitaji ushirikishwaji wa wadau
na kwa kulitambua suala hilo Serikali iliandaa
kongamano hilo ili kuisaidia kutekeleza mipango yake kwa ufanisi kupitia Mpango
wa Matokeo Makubwa Sasa.
Aidha
Waziri Ghasia alisema katika kipindi cha miaka 50 ya utumishi wa Muungano,
Serikali imechukua hatua mbalimbali za kuimarisha sekta ya utumishi wa umma
ikiwemo ubunifu wa Sera mbalimbali zinazotekelezwa kupitia kamati za
mashauriano baina ya pande mbili za Muungano.
Waziri
Ghasia aliongeza kuwa zipo changamoto mbalimbali za kimaendeleo zinazolikabili
taifa, ambapo kwa kiasi kikubwa utatuzi wake unategemea namna sekta ya utumishi
wa umma ilivyojipanga na kutekeleza wajibu wake.
“Sekta
binafsi, Asasi za Kiraia na Sekta isiyo rasmi ni sekta muhimu kwa maendeleo ya
Taifa kuweza kukaa pamoja na kubadilishana mawazo na uzoefu katika maeneo yetu,
na zote kwa pamoja zina mchango mkubwa kwa kuwa zinasaidia kuwasilisha mawazo
ya jamii Serikalini” alisema Waziri Ghasia.
Aliongeza
kuwa mwaka 2011 Serikali ilibuni sera ya ushirikiano baina yake na sekta
binafsi yaani Private Partnership Policy iliyopitishwa mwaka 2010 na kufuatiwa
na sheria ya kutekeleza sera hiyo na kwa upande wa Asasi za kiraia upo mwongozo
wa kushirikiana na asasi hizo uliotolewa mwaka 2012.
Akizungumzia
suala la maadili katika utumishi wa Umma, Waziri Ghasia alisema wapo baadhi ya
watumishi wanaokiuka maadili ya kazi ingawa si wote, kwani kwa sasa Serikali
inatafakari changamoto na mapungufu mbalimbali yaliyojitokeza katika kipindi
cha miaka 50 ya utumishi wa Umma nchini.
Kwa
upande wake Kaimu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma,
Hab Mkwizu alisema maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma ni maonesho ya wazi
na yanahudhuriwa na wananchi wote yanayotoa fursa kwa watoa huduma a,bao ni
taasisi za umma kukutana moja kwa moja na wateja na wananchi kwa upande
mwingine.
“Utaratibu
huu unatumika kuelimisha na kuonesha aina ya huduma zinazotolewa na watumishi
wa umma kwa wananchi” alisema Mkwizu.
|
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni