HOPE SERVICE STATION

nsekwa

ALTEZA

Jumanne, 20 Mei 2014

MANISPAA YA IRINGA YAJIPANGA KUONGOZA KWA USAFI


Manispaa ya Iringa imejipanga vizuri katika kuhakikisha mwaka huu inashika nafasi ya kwanza katika mashindano ya afya na usafi wa mazingira ngazi ya Taifa.
 
Akizungumza na mtandao huu wa www.mwandishiwetublog ofisini kwake leo Mganga mkuu wa Manispaa ya Iringa Daktari May Alexander alisema kuwa katika kipindi hiki Halmashauri ya Manispaa ya Iringa ipo katika mikakati ya mwisho ya kushiriki mashindano ya usafi wa mazingira na afya katika ngazi ya Kitaifa katika mwaka 2013/2014 ambapo mashindano hayo yanaratibiwa na Wizara ya Afya pamoja na Ustawi wa Jamii yakishindanisha ngazi nne ambazo ni Halmashauri ya Wilaya, Miji, Manispaa pamoja na Majiji ambapo mashindano hayo hufanyika kila mwaka na katika kila mkoa.
 
Dakatari May alisema lengo kuu la kushindanisha mashindano haya ya usafi ni kuleta 
msukumo wa kufanya miji iwe misafi ambapo Iringa imekuwa ikifanya vizuri kila mwaka ambapo iliweza kushika nafasi ya pili katika vipindi mfulululizo huku nafasi ya kwanza ikichukuliwa na jiji la Moshi.
 
“Iringa imekuwa ikifanya vizuri kwa kushika nafasi ya pili kwa mfululizo kati ya Halmashauri kumi na nane hata hivyo mwaka huu Halmashauri imeendelea na mikakati ya kuboresha usafi kwa kusimamia huduma za usafi wa mazingira yanayotuzunguka ambapo tumekuwa na vigezo tunavyotumia katika ufanyaji usafi kama kuondoa takataka zinazozalishwa majumbani, stendi, masoko na Taasisi mbalimbali, sisi kama halmashauri tumejipanga vizuri tuna magari mawili kwa ajili ya kusafilishia taka kutoka maeneo hayo na kuyapeleka dampo pia tumesambaza makontena ya kuwekea taka maeneo mbalimbali ya manispaa yetu” alisema Daktari.
Pia alisema takwimu inaonyesha wakazi wa Manispaa ya Iringa huzalisha tani 108 za taka ngumu kila siku ambapo kati ya hizo tani 48 zinatoka katika makazi ya watu, tani 33 kutoka katika biashara na viwandani, tani 21 kutoka katika masoko, stendi na maeneo ya wazi na tani 6 zinatoka katika taasisi mbalimbali hivyo halmashauri imejenga vizimba vya kuhifadhia taka katika baadhi ya maeneo ambapo kwa siku halmashauri inaweza kuondoa taka kwa wastani wa asilimia 76 za taka.
 
“sisi kama halmashauri tumejiwekea utaratibu wa uzoaji taka ambapo tunatumia njia tatu ambazo moja ni kupitia vikundi vinavyojishughulisha na usafi ambapo wao huchukua taka kutoka kwa wazalishaji na kuzipeleka katika sehemu za kuhifadhia taka yani kwenye yale makontena, pili kwa maeneo yaliyopo pembezoni mwa mjini kama maeneo ya Nduli, Igumbilo, Kitwiru, Itamba, Mgongo na Mkoga wananchi wa maeneo hayo tunawashauri wachimbe mashimo ya kuhifadhia taka ambapo zikijaa nyingine zinachoma na mwingine anaweza akafukia shimo hilo na kuchimba shimo lingine kwa ajili ya kuhifadhia taka hizo, na njia ya tatu tumeweka mapipa ya kuhifadhia taka ambazo zinapatikana maeneo ya stendi na baadhi ya maeneo ya barabara ambapo wananchi hutupa taka zao kwenye mapipa hayo na baadae yakishajaa tunayachukua na kuyapeleka katika makontena tayari kwa kupelekwa dampo” alisema.
 
Mpaka sasa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa imeshakarabati makontena kumi ambayo yalikuwa yameharibika, imejenga uzio katika makaburi ya makanyagio, imeweza kushindanisha mitaa na kata 16 zote zilizopa katika manispaa na kupitia mashindano hayo walipatikana washindi ambapo mshindi wa kwanza ni kata ya Gangilonga ikifatiwa na Mlandege nay a tatu ni Kitanzini, pia imeweza kuanzisha vikundi vinavyojishughulisha na usafi katika kata nne na imeweza kununua gari la kubebea taka litakaloingia mda wowote kuanzia sasa ambapo gari hilo limegharimu taklibani milioni 280 pia halmashauri imeweza kukarabati gari la unyonyaji maji taka ambalo wakati wowote kuanzia sasa litaanza kufanya kazi na pia ikokatika hatua za mwisho za ukamilishaji wa machinjio ya kisasa ambayo yanatarajiwa kuanza kutumika hivi karibuni.
 
Hata hivyo mashindano hayo yanatarajiwa kuanza wiki ijayo kwa hapa manispaa ya Iringa ambapo Daktari May ametoa wito kwa wakazi wa manispaa hii kuhakikisha wanayafanyia usafi maeneo yanayowazunguka na pia kutoa ushirikiano kwa maafisa afya pindi wanapopita kuwashauri juu ya kufanya usafi.
NA DIANA BISANGAO WA MATUKIO DAIMA.COM, IRINGA.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni