HOPE SERVICE STATION

nsekwa

ALTEZA

Jumapili, 18 Mei 2014

UTALII UANZE NA VYOMBO VYA HABARI NCHINI

                                      Twiga  akinywa maji 
 Twiga  akila  matawi ya  miti

Kiboka  akiwa katika mto  Ruaha mkuu 
 Tembo wakivuka katika  mto  Ruaha  mkuu hivi karibuni
MKAKATI  wa  kukuza utalii  wa ndani katika  hifadhi  za  mikoa  ya nyanda za juu ikiwemo hifadhi  ya Taifa  ya  Ruaha ukianza na vyombo  vya  habari  vya  habari nchini  utalii  wa ndani utakuwa kwa kasi na  kuwakomboa  vijana  wengi wasio  na ajira.

Ifahamike  kuwa  utali  ni  sekta mojawapo inayoweza kuwakomboa  wengi  hasa  vijana  wasio na ajira  iwapo  uhamasishaji  utafanyika  katika  vyombo vyetu  vya habari zikiwemo radio  za kijamii ambazo ndizo  zinasikilizwa zaidi  na  vijana  walio wengi ambao  hupenda  kusikiliza radio hizo kutokana na muziki inayopigwa muda  mwingi  zaidi.
 
John Moleli ni  mmoja kati  ya  vijana  ambao  wamepata  kujiajiri wenyewe  katika  sekta  ya utalii kuwatembeza watalii katika maeneo mbali mbali  ya mji  wa Iringa  pindi  wanapofika   kutembelea  hifadhi  ya  Ruaha Iringa na baadhi ya maeneo  ya  vivutio  vya utalii yakiwemo makumbusho  ya chifu Mkwawa  eneo la Kalenga .

Moleli  anasema  kuwa tatizo  la vijana  wengi  kutojiingiza katika shughuli ya utalii  ndani ya  mikoa ya  kusini ni kutokana na  kutokuwa na elimu ya  kutosha  ya utalii   na  wale  wachache ambao  wanafanya shughuli  za kitalii kwa maana ya kuuza vinyago mbali mbali na  kufanya kazi  ya  kuwatembeza  watalii katikati ya  mji  wa Iringa ni  wale  ambao  wametokea  mikoa ya  kaskazini kama Arusha , Kilimanjaro  na  Msoma ambako   sekta  ya  utalii imeonyesha  kuwa  kimbilio  la vijana  wengi.
 
“ Mfano  vyombo  vya habari  vya  mikoa ya kaskazini  vimefanya kazi kubwa  ya kutangaza utalii  na vijana  wengi  kupitia  elimu mbali mbali  inayotolewa na  vyombo hivyo  vya habari  walipata  kuhamasika  na  kupenda shughuli  za kitalii ….japo  jambo  jingine  ambalo limefanya  vijana  wengi wa mikoa ya kaskazini  kuwa na ajira ya uhakika katika  sekta ya utalii ni wao wenyewe  kuupenda utalii  na kujikuta  wengi  wao  badala ya  kushinda vijiweni ama stendi kufanya kazi ya kupiga debe katika  vyombo vya usafiri  kwa kipato kidogo wamekuwa wakielekeza nguvu  zao kupigia debe sekta ya utalii kwa kuuza bidhaa mbali mbali ama kuongoza  watalii“ alisema
 
Kuwa kutokana  na  hesima  kubwa iliyopo  mkoa  wa Iringa  kwa  kuwa na hifadhi  kubwa  kuliko  zote nchini hifadhi ya  Ruaha na kama vyombo  vya  habari na  wanahabari mkoa  wa Iringa  watatumia  vema kalamu zao  kuitangaza hifadhi  hiyo ikiwa ni  pamoja  na kuandaa vipindi vya elimu ya utalii na jinsi ya vijana  mkoani Iringa wanavyoweza kujiajiri  wenyewe katika sekta   hiyo  ni wazi  wageni  wa ndani na nje  watakaofika mkoani Iringa  kutembelea  hifadhi hiyo  watakuwa ni sehemu ya  ajira ya uhakika kwa vijana.
 
“Binafsi nashangazwa na vyombo  vya habari  vya utangazaji mkoani Iringa mbali ya kuwa ni moja kati ya mkoa wenye idadi kubwa  ya radio kwa  kufikia idadi  ya vituo vya radio na Runinga zaidi ya 6 ila  bado  sehemu kubwa  ya vituo  hivyo  vya radio  vimekuwa  si msaada wa  kutangaza utalii  wa kusini kutokana na kutenga muda mwingi wa  burudani badala ya kutenga muda wa  kuelezea utajiri mkubwa ambao mkoa wa Iringa unao ambao pia ungewezesha vituo hivyo  kunufaika  utajiri wa vivutio  vya utalii na utalii wa ndani kwa watanzania  hasa wakazi wa mkoa wa Iringa  wenyewe”
 
Kwa  upande  wake Musa Simoni Onesmo   ambae ni  mmoja kati ya  wanachama  wa  chama cha Iringa Masai Market anasema  katika mkoa wa Iringa utalii ndio umeanza kuonekana  miaka  ya hivi karibuni hasa  wakati  wanafanyia  shughuli hiyo   eneo la Posta kabla ya uongozi  wa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa  kuwatoa eneo hilo ambalo lilikumbwa na mkasa wa kuungua moto miaka miwili  iliyopita  hivyo wao  kuamua kujibanza eneo la IDYDC  kando  ya  barabara  ya Uhuru kati  ya Iringa – Dodoma .
 
Anasema kuwa  eneo  hilo bado  si la  kuutangaza  utalii  kwani biashara ya vinyago ambayo  wanaifanya inahitaji eneo linaloonekana   vizuri kwa watalii kama eneo la Bustani  ya Manispaa ya  Iringa ama eneo jingine linaloonekana  vizuri  tofauti na hapo  walipo ambapo ni mafichoni  zaidi.
 
Hata  hivyo anasema  kuwa kwa upande wake  ameanza shughuli  hizo  za kuuza vinyago kwa watalii zaidi ya  miaka 10  sasa na hamasa ya kuanza shughuli  hiyo aliipata  kutoka kwa kaka zake ambao  walikuwa wakimtuma shughuli za kuuza vinyango kwa watalii katika mkoa wa Arusha na  sasa ameanzisha  biashara yake  mwenyewe .
 
Huku akidai  kwa mkoa wa Iringa kasi  ya wateja wa bidhaa za kitalii ni ndogo sana ukilinganisha na mikoa ya Kaskazini  japo ni  kubwa kwa  sasa ukilinganisha na miaka ya 2000 na 2010 katika  mkoa  huo  wa Iringa na  kuwa hivi  sasa hata watalii wa ndani ambao  awali  walikuwa  wakipuuza vinyango kwa  sasa  wanafika  kununua bidhaa hizo  za kitali japo  bei wanayouziwa  watalii wa ndani ni chini  na ile ya  watalii wa nje.
 
Victor Chakudika ni meneja  wa  kituo cha Radio Nuru Fm  ambacho ni kituo cha radio ya jamii kwa mikoa ya nyanda za juu  kusini anasema  kuwa wao kama radio ya kijamii wameanza kuhamasisha utalii wa ndani na sekta nzima ya utalii katika mkoa  wa Iringa.
 
Chakudika anasema  kuwa wameanzisha  vipindi  mbali mbali vya kijamii  kikiwemo kipindi cha kuhamasisha utalii pamoja na kutoa  elimu kwa wananchi juu ya faida ya utalii ambapo  wamekuwa  wakiwaalika  wadau mbali mbali wa sekta ya  utalii nchini.
 
Mstahiki  meya  wa Halmashauri  ya Manispaa  ya  Iringa Aman Mwamwindi akizungumzia  suala la  ukuzaji utalii  wa ndani  katika Manispaa ya  Iringa amesema  kuwa ushauri  wa  vijana  hao ameupokea japo kwa  sasa eneo hilo la bustani ya Manispaa ya Iringa imechukuliwa na mwekezaji mwingine kwa ajili ya kupatunza  zaidi kwa  kuuza vinywaji  baridi .
 
Kwani anasema  tenda ya  kuendesha eneo hilo ilitangazwa na vijana  hao hawakuomba ila kutokana na mkakati wa  serikali ya mkoa wa Iringa  kuelekeza nguvu katika sekta ya utalii wa ndani na nje Manispaa ya Iringa itafanya mazungumzo  na mwekezaji  wa  eneo  hilo  ili biashara  za bidhaa za kitalii  kuwepo pia eneo hilo.
 
Ofisa Utalii wa Tanapa wa ofisi ya Utalii Kanda ya Nyanda za Juu Kusini Bi Risala Kabongo anasema  kuwa ofisi yake imeanza mkakati  wa kuhamasisha  utalii wa ndani katika hifadhi za mikoa ya nyanda zakanda ya nyanda za juu  kusini ikiwa ni pamoja na  kukutana na  watoa  huduma mbali mbali  wakiwemo wa mahotel   na kuwapa  elimu ya kuwahudumia  wageni .
 
Kwani  anasema  kuwa  sekta  ya utalii itakuwa zaidi  iwapo watoa huduma  mbali mbali  watakuwa na elimu juu ya huduma  wanazozitoa  kwa  wateja  wao  wakiwemo  watalii
Huku akiwataka  vijana kutumia vema  sekta ya utalii hata kwa kujipanga  kuwatembeza watalii pindi  wanapokuja katika mji wa Iringa kwa ajili ya kwenda katika vivutio vya utalii.
 
Bi Kabongo anasema  kuwa sehemu kubwa ya  watalii wamekuwa  wakitembea wenyewe katika mitaa ya mji wa Iringa  bila ya mwenyeji  jambo ambalo halifai .
  
Kaimu Mkurugenzi  mkuu wa TANAPA ambae  ni mkurugenzi wa mipango na Utalii wa Tanapa, Dk Ezekiel Dembe anasema kuwa idadi  ya  watalii wa ndani na nje wanaotembelea hifadhi ya Ruaha na hifadhi nyingine nchini ni kubwa  zaidi japo lengo  ni kufikisha watalii milioni 2.5 hadi  mwaka 2015.
 
Anasema  kuwa lengo ni kuona idadi ya  watalii  katika hifadhi  inakua  kwa kuzingatia ubora sio ukubwa ili kulinda ikolojia ya maeneo yaliyohifadhiwa
 
Dr Dembe anasema  kuwa kasi  ya  watalii wa nje katika  hifadhi ya Ruaha mbali ya  kuwa inazidi  kuongezeka mwaka  baada ya mwaka  ila  changamoto kubwa ni kutokuwepo kwa mafuta  ya ndege katika  uwanja  wa Nduli Iringa  jambo ambalo  linawalazimu  watalii kujaza mafuta Dodoma kabla ya kwenda Iringa .
 
Hivyo TANAPA inafanya mchakato  wa  kuwatapa  wawekezaji  watakaouza mafuta ya ndege Msembe   katika  hifadhi ya  Ruaha na Katavi pamoja na  kuwapata  wawekezaji watakaowekeza katika  sekta ya Lodge na Hotel katika hifadhi  hizo.
 Hifadhi ya Taifa  ya  Ruaha yenye  ukubwa wa kilomita  za mraba 20,226 ni hifadhi kubwa   kuliko zote nchini nay a pili kwa ukubwa katika Afrika baada ya hifadhi ya Kafue nchini Zambia
 
Sehemu  kubwa ya  watalii wa nje na  wandani  hupenda kutembelea  hifadhi  hii kutokana na kuwa na umaarufu wa wanyama aina ya kudu  wakubwa na wadogo ambao hupatikana kwa  wingi katika hifadhi  hii  huku  ustawi wa hifadhi hii ukitegemea  mto   Ruaha mkuu.
Mandhari ya hifadhi ya Ruaha ni mazuri kwa watalii wa ndani na  watalii wa nje na hifadhi  hii  inafikika  vizuri  kutokana na miundo mbinu yake mizuri .
 
Hifadhi  ya  Ruaha  ipo katikati ya Tanzania umbai  wa kilomita 128 Magharibi mwa mji wa Iringa na inafikika pia kwa usafiri  kwa ndege  za kukodi  huku magari  hufika  wakati wote wa  mwaka  kutoka Dar es Salaam ni kilomita 625,Mikumi , Iringa na Arusha  kwa  kupitia Dodoma.
 
Mbali  ya hifadhi ya Ruaha Iringa Tanzania tunajivunia kwa kuwa na hifadhi kama Serengeti  Udzungwa ,Mlima Kilimanjaro, Tarangire, Manyara, Arusha, Mkomazi, Mikumi,, Katavi, Kitulo,  pamoja na  vivutio vingine  kwa mkoa wa Iringa kama kisima  cha  Mkwawa ,maskani ya  watu wa kale  katika  kijiji  cha Ismila  umbali wa kilomita 120 kutoka Iringa mjini na vivutio vingine vingi .

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni