Jeshi
la Magereza litafanya Maadhimisho ya Siku ya Magereza Nchini tarehe 20
Juni, 2014 kuanzia saa 2:00 asubuhi katika Viwanja vya Chuo cha Maafisa
wa Magereza Ukonga, Dar es Salaam ambapo Mgeni rasmi anatarajiwa kuwa
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. Mathias Chikawe(MB).
Kwa mujibu wa taarifa rasmi
iliyotolewa leo Juni 18, 2014 na Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza,
John Casmir Minja Maadhimisho haya ni ya pili kufanyika tangu Jeshi la
Magereza Tanzania lianzishwe rasmi mwaka 1931. Madhumuni ya Siku ya
Magereza ni:-
a) Kuelimisha jamii juu ya shughuli mbalimbali zinazofanywa na Jeshi la Magereza katika
utekelezaji wa majukumu yake ya uhifadhi na Urekebishaji wa wahalifu kupitia shughuli za
viwanda Vidogo Vidogo, Ujenzi, Kilimo, Ufugaji na Ufundi katika fani mbalimbali.
b) Kuelimisha na kuhamasisha jamii juu ya umuhimu wa kushiriki kikamilifu katika suala zima la
Urekebishaji wa wahalifu na;
c) Kutoa elimu kwa umma juu ya huduma na taratibu za Uendeshaji wa Magereza Nchini.
Shughuli zitakazofanyika siku
hiyo ni pamoja na ufunguzi wa Duka la Bidhaa zisizolipiwa Kodi (Duty
Free Shop) Gereza Keko, kukagua shughuli zinazofanyika kwenye Ofisi za
Chama cha Ushirika wa Kuweka na Kukopa kwa Watumishi wa Jeshi la
Magereza (TPS SACCOS) eneo la Keko, kufungua Karakana ya Uhunzi Gereza
Ukonga, Gwaride Maalum, Onesho kutoka Kikosi Maalum la utayari wa
Kutuliza Ghasia Magerezani. Ushuhuda wa Mfungwa aliyepata Shahada ya
Sheria (LLB) akiwa gerezani, Burudani Maalum ya muziki kutoka kwa
wafungwa, askari wa kike waliohitimu mafunzo maalum kukabidhiwa vyeti na
Mgeni rasmi na maonesho ya kazi mbalimbali zinazofanywa na Jeshi la
Magereza.
Vyombo vya Habari na Wananchi
wote wa Mkoa wa Dar es Salaam na Mikoa jirani wanakaribishwa kuja
kushiriki katika Maadhimisho haya ili wapate nafasi ya kuona na
kujifunzia shughuli mbalimbali zinazofanywa na Jeshi la Magereza.
Imetolewa na;
Lucas Ambrose Mboje, Mkaguzi wa Magereza,
Afisa Habari Makao Makuu ya Jeshi la Magereza,
18 Juni, 2014,
DAR ES SALAAM.
Lucas Ambrose Mboje, Mkaguzi wa Magereza,
Afisa Habari Makao Makuu ya Jeshi la Magereza,
18 Juni, 2014,
DAR ES SALAAM.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni