WASAILIWA 1,281 KUINGIA DURU YA MWISHO YA USAILI WA NAFASI YA MKAGUZI MSAIDIZI WA UHAMIAJI (ASSISTANT INSPECTOR OF IMMIGRATION)
Wasailiwa 1,281 kati ya 6,115
waliofanya usaili wa kwanza tarehe 13 Juni, 2014 jijini Dar es Salam
kuomba nafasi ya Mkaguzi Msaidizi wa Uhamiaji (Assistant Inspector of
Immigration) wanatarajiwa kuingia duru ya pili na ya mwisho ya usaili
huo baada ya kufanikiwa kufaulu usaili wa kwanza.
Usaili huu ambao utafanyika kwa
awamu utaanza tarehe 23 Juni hadi 03 Julai, 2014 na utafanyikia katika
Bwalo la Maafisa Magereza, Ukonga jijini Dar es Salaam kuanzia saa 1.30
asubuhi.
Tofauti na usaili wa kwanza ambao
ulikuwa wa kuandika na ulihusisha maswali ya hesabu na ufahamu wa jumla,
usaili wa awamu ya pili utakuwa wa maswali ya ana kwa ana ambao
utahusisha kupima uwezo wa msailiwa kujieleza na kufafanua mambo.
Kuchaguliwa kwa wasailiwa hawa
kulifanyika baada ya kusahihisha majibu yao na majina kuingizwa katika
mfumo wa kimtandao ambao ulisaidia kuchagua wasailiwa waliopata alama
hamsini na kuendelea.
Majina ya wasailiwa hawa yanapatikana katika Tovuti ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, www.moha.go.tz na ya Idara ya Uhamiaji, www.uhamiaji.go.tz na watatakiwa kuja na vyeti vyao halisi vya kuzaliwa, vya shule na picha mbili za pasipoti.
Awali, kiasi cha
wasailiwa 10,801 waliitwa kwa ajili ya usaili wa kwanza baada ya kupokea
maombi yao, lakini waliohudhuria ni 6,115 na kati yao ndio walipatikana
1,281 ambao watasailiwa ili kupata watakaojaza nafasi sabini (70) za
Mkaguzi Msaidizi wa Uhamiaji katika Idara ya Uhamiaji.
Sgn
Isaac J. Nantanga
0754 484286
MSEMAJI,
WIZARA YA MAMBO YA NDANI YA NCHI
18 Juni, 2013
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni