HOPE SERVICE STATION

nsekwa

ALTEZA

Jumamosi, 24 Mei 2014

VIONGOZI WA SERIKALI YA KIJIJI CHA IBUMU MATATANI KWA KUHARIBU VYANZO VYA MAJI


WANANCHI wa kijiji  cha Ibumu katika  wilaya ya  Kilolo mkoani Iringa wamewatuhumu  viongozi  wao wa   serikali ya kijiji  hicho  kuwa ni vinara  wa ulimaji katika  vyanzo vya maji .

Wakizungumza katika  mdahalo  wa  usimamizi shirikishi wa raslimali maji ,misitu na fedha  za umma ulioandiliwa na asasi ya  kiraia ya MMADEA  juzi  wananchi  hao  walisema  kuwa  sehemu kubwa ya  wananchi  wa  kijiji  hicho  wanaendesha maisha yao  kupitia kilimo cha maeneo  yenye maji maarufu kama  vinyungu wakiwemo  viongozi  wa serikali ya kijiji  hicho.

Hivyo  kitendo  cha asasi ya MMADEA kufika  kijijini hapo kwa ajili ya  kuunda mtandao  wa kusimamia rasilimali  hizo  ikiwemo ya maji na misitu  viongozi  hao  waliona ni kama mwiba  kwao kutokana na kuwa  wao  wenyewe  ndio  wanaoongoza  kwa  uharibifu  wa mazingira  katika maeneo ya vyanzo  vya maji.

Wananchi hao  waliomba MMADEA kwa  kushirikiana na  serikali ngazi ya  wilaya  kuweka mkakati wa pamoja na  kulinda vyanzo vya maji  kwa faida ya  vizazi vijavyo  badala ya kuendelea  kuwafumbia macho  viongozi  wa  serikali ambao  hawapo tayari  kulinda  vyanzo  hivyo  vya maji.

Mbali ya   kuwataka  viongozi hao  kubanwa kwa  kushindwa  kulinda  vyanzo vya maji  bado  wananchi hao  walisema  kumekuwepo na usimamizi mbaya wa  fedha  za umma  zinazotolewa  katika  kijiji hicho kwa ajili ya  shughuli  na maendeleo .

" Tunashangazwa sana na  viongozi  wetu  wa  serikali  kushindwa  kushirikia nasi katika mdahalo  huu na  kukimbia wakati lengo la MMADEA ni  kwa faida  yetu  wenyewe .......sasa  tunaomba hatua  zichukuliwe kwa  viongozi  wetu  ambao  watabainika  kuwa  sehemu ya uharibifu  wa mazingira  katika  vyanzo  vya maji "

Hata  hivyo  vingozi hao  mwenyekiti na mtendaji  wa  kijiji hawakuweza  kupatikana  kuzungumzia tuhuma   hizo  dhidi yao  huku  mmoja kati ya  wajumbe wa  serikali ya  kijiji  hicho ambao aliomba jina  lake  kuhifadhiwa  kwa  kuwa  si msemaji  wa serikali  ya kijiji  hicho  ,alisema  kuwa  mwenyekiti  wa kijiji na mtendaji pamoja na diwani  wao ni miongoni  mwa wananchi wanaolima katika vyanzo vya maji na ndio  sababu ya  kushindwa  kufika katika mdahalo  huo.

Pia  alisema viongozi  hao  ndio  waliopanga  vijana  kuvuruga  mdahalo  huo uli  usifanikiwe  kama  njia ya kuficha suala  hilo la wao  kulima katika  vyanazo  vya maji.

Mkuu  wa  wilaya ya  Kilolo Gerald  Guninita  alisema kuwa  zipo  sheria  zinazoelekea  mita za kulima  kutoka katika  vyanzo vya maji na kuwa  serikali ya  wilaya  hiyo haitakuwa tayari  kuona  wananchi  wakilima katika  vyanzo vya maji na hivyo kuwataka  viongozi  na wananchi  wanaoendelea  kulima katika vyanzo hivyo  kuondoka wenyewe kabla ya  kuwajibishwa kwa mujibu wa  sheria.

Mratibu  wa MMADEA  mkoa  wa Iringa Raphael Mtitu  alisema  kuwa mdahalo huo  ulilenga  kuwaelimisha  wananchi ili  kuweza  kushiriki katika uhifadhi wa misitu na maji katika maeneo yao .

Alisema  kuwa asasi  hiyo  imekuwa  ikifanya kazi katika tarafa ya Mahenge na Mazombe katika  wilaya ya  Kilolo pia  alisema  faida  kubwa ya  uhifadhi  wa mazingira  ni pamoja na  wananchi hao  kupata  mvua ya  kutosha na kuweza  kukabiliana na mabadiliko ya tabia  nchi  ambayo  yameendelea  kulikumba Taifa na  dunia kwa ujumla .
MWISHO

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni